Tuesday, March 26, 2013

NJAMA

SURA YA KUMI

"UHURU UTALETWA KWA MTUTU TU"

Tulipoingia ofisini tulikuta wanatusubiri kwa hamu.

"Chifu anataka kukuona", Eddy alinieleza.

"Mwambie Maselina haiwezekani, nitamwona baadaye. Sasa hivi hakuna nafasi maana tukichelewa hapa mambo yote yatakuwa yameharibika. Mwambie asitoke ofisini mpaka saa sita. Asipotuona ajue basi makubwa yametupata, akituona ajue tumerudi na ushindi. Umesikia Linda?".

"Nimesikia".

"Sherriff, Eddy na Isaack mko tayari kwenda kwenye uwanja wa mapambano", niliwauliza.

"Bila wasiwasi", walijibu kwa pamoja.

"Na mimi?", Zabibu aliuliza.

"Wewe utabaki hapa na Linda. Tutaonana saa sita kama tukiwa salama.

"Mimi nataka twende wote, kama ni kufa tukafe wote"

"Kwanini unataka ukafe naye kwani yeye ni nani wako", Linda alimuuliza kwa ukali.

"Acheni upuuzi, nyinyi bakini hapa, haya mambo ya kuleteana haraha, mtatupa mkosi bure".

"Twendeni zetu", niliwaeleza wenzangu nasi tukaondoka ndani ya ofisi na kuingia ndani ya gari.

Eddy ndiye alichukua usukani na Isaack akaa naye mbele. Mimi na Sherriff tulikaa nyuma.

"Twende moja kwa moja nyumbani kwangu tukachukue silaha zaidi. Halafu tutapita nyumbani kwa Eddy kuchukua silaha tulizoacha kule. Tuna saa moja ya kujitayarisha kabla ya kuingia kwenye uwanja wa mapambano.

"Itabidi tutoke kwa Eddy mnamo saa tatu na nusu. Hii itatupa nafasi ya kuwa nje ya nyumba ya Sikazwe saa tatu na nusu. Maana ndipo yeye ataondoka kuelekea huko walikoziweka silaha".

"Kisha niliwaeleza mazungumzo yote niliyoyasikia kati ya Harrison, Sikazwe na Max.

Kwa hiyo tutakuwa watu wanne tukikabiriana na zaidi ya watu mia", Isaack alisema kwa mshangao.

"Ndiyo sababu watu kama sisi tunaitwa ni hatari. Siku moja Isaack utakapokuwa komando kama mimi utakuwa na uwezo wa kukabiliana na maadui mia peke yako. Kwa hiyo mimi naona kama ni afadhali sana kama tuko watu wanne dhidi ya watu mia. Tukitumia hamasa na maadili na moyo wa kimapinduzi sina shaka Mungu atatusaidia na tutashinda na kufichua hizi njama za Makaburu na mabeberu ya jumuia ya ulimwengu", niliwatia moyo.

"Nikiwa niko na wewe bosi, huna sina wasiwasi wowote", Eddy alisema.

"Hata mimi", Sherriff aliongeza.

"Kama ni hivyo, hata mimi ninafurahi kuwa nina jeshi lililohai na kamanda wake".

"Kutokana na ulivyoeleza komredi, watu hawa walikuwa wamepanga kuzichukua silaha hizi kwa meli ndogo kama spea ziendazo Mtwara", Sherriff alieleza.

"Sawa'.

"Baada ya kufika Mtwara wangefanya nini?", aliuliza.

"Swali zuri. Watu hawa walikuwa wamejitayarisha vizuri sana. Hili kampuni kubwa la Euro-Afro lina meli zake. Meli yake moja itakuwa inapakua mizigo Mtwara kuingia kesho. Hivyo walikuwa wamepanga kutoa silaha hizi kwenye hii meli ndogo na kuzipakia katika meli kubwa ambayo ingelikwenda kuzitelemsha Afrika Kusini...

"Mipango yote hii iko ndani ya faili nililompa Linda ampelekee Chifu. Meli hiyo ingekuwa inangojwa bandari ya East London kutelemsha zana hizi. Sikazwe angeondoka kesho kwa ndege akidai anakwenda Botswana lakini angekwenda Pretoria ambako mimi nafikiri wangemtia ndani mana nia yao haikuwa kufanya kama walivyomdanganya ila tu walitaka awasaidie kuziiba silaha kwa sababu ilikuwa rahisi kwake".

"Kwa hiyo mpaka sasa Sikazwe anakazana bure tu", Isaack alisema huku akicheka.

"Wajinga ndio waliwao", Eddy alijibu. Tulifika nyumbani kwangu, nikabadilisha mavazi kuvaa mavazi ya kikazi yaani koti na suruali yenye mifuko mingi ili kuweza kubeba silaha za kutosha.

Baada ya hapo tukaelekea kwa Eddy ambako tulijitayarisha kwa kikamilifu. Kwa bahati nzuri tulikuwa na majoho mekundu matano tuliyoyateka kwa hawa majahili. Kila mtu alichukua joho moja, maana hii ingetusaidia kuwaingilia wakidhani ni wenzao. Tulipata vile vile kofia tatu ambazo niliwagawia wenzangu. Nakwambia tulipojaribu kuvaa tulifanana na wao kabisa. Hivyo tulichoomba ni kuwa tukute bado hawajabadili mvao wao unaowatambulisha. Baada ya kuona kila kitu kimekamilika tulijiandaa kuondoka huku roho zetu zikipiga haraka haraka.

II

Ilikuwa saa tatu na dakika ishirini tulipoegesha gari yetu kando kando ya bahari huku tukiangalia nyumba ya Sikazwe. Tulimsubiri aanze safari yake hapo saa tatu na nusu. Gari lake lilikuwepo hivyo tuliamini yupo.

Saa tatu na nusu kamili kama alivyosema tuliona mlango wa mbele wa nyumba unafunguliwa Max ndiye alitoka kwanza akiwa amevalia joho jekundu na kofia. Roho yangua ilijawa na furaha. Baada ya muda kidogo Sikazwe akiwa amevaa suti nyeupe alitoka akafunga mlango, halafu wote wawili wakaingia ndani ya gari. Max ndiye aliyeingia upande wa dereva. Sikazwe akaa kwenye viti vya nyuma.

"Lo Sikazwe ameanza kupata heshima ya "VIP", Sherriff alisema na wote tukacheka.

"Yule aliyetoka kwanza alikuwa Max; anaonekana ndiye Kamanda wa jeshi hili la majahili, na haikosi ndiye aliyekwenda bandarini kama Meja Paul Liboi", niliwaeleza

"Bila shaka", alijibu Sherriff.

"Hamna taabu bosi".

Gari la Sikazwe liliondoka na kuingia Kenyatta  Drive. Tulingoja mpaka lilipofika kwenye kona ya Barabara ya Bagamoyo ndipo tukamfuata. Nakwambia mimi nikimfuata mtu hata awe na ujuzi wa namna gani hawezi kutambua. Tulifuatana moja kwa moja wakashika barabara ya Upanga, halafu wakaingia barabara ya Azikiwe kisha wakaingia Azania Front na kutokea City Drive. Muda wote huu sisi tuliwafuata taratibu.

Kisha walishika barabara inayopita kwenye ofisi za usalama barabarani nikajua wanaelekea Kurasini. Nilishangaa kwanini hawakupita Intercontinental Motors kama walivyokuwa wamepanga, lakini nilihisi wamebadilisha mipango.

Walipovuka tu ofisi za polisi wa usalama barabarani, walisimama. Mara mtu akatokea kwenye kijinjia akaja na kuzungumza nao. Mimi niliwapita kasi mpaka kwenye mzunguko wa barabara hii na barabara ya Kilwa, Nikazungukia kulia na kuingia Railway Clab na kutoka. Sisi tukawa kama tunatokea mtaa wa Gerezani. Niliendesha polepole na mara nikawaona wanatokeza kuelekea barabara ya Kilwa nasi, tukawafuata.

Tulipofika kwenye njia panda ya Kilwa na barabara iendayo kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandari ya Tanzania wao walichukua njia iendayo kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandri.

"Nafikiri wamezificha Shimo la Udongo", alisema Isaack.

"La hasha, mbele ya ofisi za NOTCO na UDA kuna bohari la Intercontinental Motors, kwa hiyo bila shaka ndiko wanakokwenda", alisema Eddy.

"Sawa kabisa Eddy, umenitoa usingizini, saa zote hizi nafikiria wapi wameficha silaha hizi kumbe sehemu yenyewe iki wazi kabisa", Sasa sikiwa na haja ya kuwafuata karibu karibu. Tuliwaacha wakaenda mpaka wakapotea kwani sisi tuliingia ofisi za Mamlaka ya Bandari, na tulipoona wamepotea ndipo sisi tukatoka.

Bohari ya Intercontinental Motors lilikuwa nyuma ya mabohari ya kampuni ya NOTCO. Hivyo niliegesha kwenye ofisi za NOTCO. Mlinzi wa hapa alikuja kutuuliza. Mimi niliona huyu anaweza kuleta kidamisi hivyo alipoinamisha kichwa kwenye gari nilimpiga ngumi ya uso ambayo ingemfanya alale kwa muda wa masaa kama manne hivi kabla hajapata fahamu. Kisha wote tulitelemka na kumbeba na kumpandisha kwenye lori moja lililokuwa limejaa mizigo.

"Haya mabohari ya NOTCO yana walinzi hivyo itabidi tuzunguke tutokee upande wa barabara ya Kilwa ili kuepusha rabusha kabla hatujafika maana jinsi tulivyo watu wanaweza kufikiri sisi ni majambazi", Eddy alitoa ombi.

"Hapana, sasa hivi bado mapema hata tukionana nao watafikiri ni walinzi wa usalama tu. Ili tuwe kwenye hali ya usalama zaidi lazima wote tuwafanye wakalale kwa muda". 

"Nami nilikuwa nafikiri hivyo maana wakisikia mapambano yatakapoanza wanaweza kuja kujiunga na kufa bure, au kupiga simu polisi wakaja kutuingilia kabla hatujafunga kazi sawasawa.

Hivyo rafiki zangu walinzi wote wa sehemu hii walilazwa usingizi wa masaa, sio wa NOTCO tu ila wa UDA, Shirika la Usagishaji na ofisi zote za karibu. Tulipoona kazi hii ndogo tumeimaliza tuliondoka hapo na kuelekea kwenye uwanja wa mapambano.

ITAENDELEA

1 comment:

  1. Harrah's Kansas City Hotel and Casino - JT Hub
    Harrah's Kansas City Hotel 속초 출장샵 and Casino - 777 Harrahs Blvd. KC, 오산 출장마사지 Missouri, 용인 출장안마 89119 US. Find reviews and discounts 경주 출장안마 for AAA/AARP members, 경기도 출장안마 seniors,

    ReplyDelete