Wednesday, February 27, 2013

NJAMA

SURA YA NANE

USIKU WA HEKAHEKA

Tulipofika Kilimanjaro Hoteli ilikuwa yapata saa tatu kamili. Tulipokuwa njiani kuelekea Kilimanjaro nilimweleza Eddy mambo yote niliyokuwa nimepata toka kwa Zabibu, mambo ambayo hata yeye alisema yalionyesha ufumbuzi wa jambo hili kwa mtu mwenye kufikiri. Tuliingia hotelini tukapanda lifti iliyotushusha orofa ya pili. Tulipotoka ndani ya lifti mara ile hali ya tahadhari ilituingia. Mimi nilitoa bastola yangu nikaiweka tayari na Eddy akafanya vile vile.

Tulipofika mlango wa chumba namba 206 tulikuta umefungwa, niligonga nikiwa nimesimama upande kabisa. Niligonga mlango mara mbili haraka haraka, halafu nikatulia kidogo kisha nikagonga tena, kwani hivi ndivyo Veronika alikuwa amenielekeza namna ya kujitambulisha lakini sikusikia kitu. Nilimonyesha ishara Eddy abane ukutani wakati mimi nafungua.

Nilifungua mlango ghafla. Tishio nililolikuta sijawahi kulipata tena, kwani Veronika alikuwa amelala kwenye sofa na kisu chenye mpini mwekundu kikiwa kimemwingia juu kidogo ya titi la kushoto. Kidogo ningezimia lakini nilijikaza nikakimbia pale kwenye sofa huku nikikanyaga maiti za watu wengine hapo chumbani.

Veronika alikuwa bado ameshikilia mkono wa simu mikononi mwake. Nilipomfikia nilimkuta bado yuko hai. Wakati huo Eddy nae alikuwa ameingia akanipa glasi ya whiski.

"Bosi jikaze, mnyweshe hii whiski mimi naita gari la hospitali"'

Nilimnywesha Veronika kisha nikamtingisha akafunua macho akapata fahamu kidogo.

"Vero, Willy hapa, niambie nani amefanya hivi".

"Walikuja.... watatu... nikapam...bana ...nikawaua nikakupigia simu.... ku...ku...kumbe walikuwepo... wengine ...wawili ... mmoja ... akamwita ... Shu... Shu...Shuta muue.... mimi kugeuka ... akanichoma... ki... kisu... nikawahi ...kumpiga yule mwingine ...kwa... akafa... Shuta... akakimbia ...nika...

Hakuweza kusema tena. Nikamwongeza whiski na kumtingisha.

"Oh Vero, nimeita gari la wagonjwa na mganga anakuja sasa hivi utapona tu.

"Si...siwezi...nitakufa...nimekufa...ame...moyo...Willy na...nakufa...na...ku...penda ...hakuna  tena... mwanamume... niliye... mpenda...kama wewe. Ni...nimefurahi...kukuona ...ma...mara... ya...mwisho...nikifa ...kwa ajili ya Afrika... siogopi...kufa...kwani nimekufa ...kwa sa...sabab...bu...nzuri. Ende...le..za ...ma...pa...mba...no... Willy ...Mungu...a...ku...sai...die...uni...ku...pi...zie...kisasi Afrika. Ni...busu...na... ku...

Nilijua Veronika hawezi kuchukua dakika moja zaidi, niliweka midomo yangu kwenye midomo yake na kulamba damu yake ambayo sasa ilikuwa inatoka mdomoni.Alitabasamu na macho yake yakang'ara kiasi ambacho sikuwahi kuyaona yanang'ara vile halafu akayapepesa akafariki. Alikufa huku akitabasamu.

Sikuwahi kulia na kupata uchungu kama wakati wa kifo cha Veronika. Nilijilaumu. Kama ningekwenda nae kwa Zabibu asingekufa.

Eddy alinikuta nabubujika machozi kama mama anayemlilia mtoto wake wa pekee.

"Bosi jikaze", Eddy alinishauri.

"Washenzi hawa, nduli hawa, watanitambua. Kwanini Mungu anaruhusu mtu kama Veronika kufa mikononi mwangu?. Eee Mungu nisaidie nilipize kisasi kwa ajili ya mwanamapinduzi huyu wa Afrika nzima", niliomba kwa sauti huku machozi yananitoka. Vero alikuwa amekufa kishujaa. Alikuwa amewaua maadui wanne pale pale chumbani.

Niling'oa kile kisu nikasafisha damu yake kwenye nguo zake.

"Kisu hiki hiki kitawauwa kama walivyomwua Veronika", nilisema.

"Bosi ninataka toka sasa tuwe pamoja".

"Hapana sasa hivi, fanya mpango wa kuondoa maiti hizi humu ndani. Na umwarifu Chifu, polisi wala wakuu wa hoteli wasiingilie. Na halafu kampashe Sherriff habari hizi za huzuni. Muushughulikie mwili wa Veronika uweze kupelekwa kwao. Mwambie Sherriff ashughulike na habari hiyo tu mambo mengine aniachie. Mwambie Chifu mambo yote yalivyo mpaka sasa mimi namfuata Shuta lazima alipe. Fanya hayo kwanza halafu nitakapokuhitaji nitakujulisha".

Niliondoka na kumwacha Eddy mle ndani ya chumba nikakimbia kwenye lifti iliyonitelemsha chini. Nilipita pale mapokezi huku nikikimbia kiasi cha watu wote kunishangaa.

Niliingia ndani ya gari Eddy alilokuwa amekodi na kuliacha Kilimanjaro Hoteli nikaondoka kwenda kumtafuta Shuta.

II

Niliondoka na kuelekea nyumbani kwa Eddy nilikomwacha Zabibu. Njiani nilifikiria uhusiano wangu na Veronika tokea siku tuliyoonana mwenye ndege mpaka kifo chake kilipotokea mikononi mwangu dakika chache zilizopita. Nilisikia uchungu usio kifani. Hasira na chuki yangu kwa makaburu, mabeberu na vibaraka wao ilizidi kiwango chake cha kila siku.

"Kifo peke yake ndicho kitaniachisha kuwawinda hawa wadhalimu maishani mwangu", niliapa.

Nilipofika nyumbani kwa Eddy nilimkuta Zabibu amekaa kwenye sofa pale tulipomwacha.

"Kumetokea nini, mbona ulikuwa unalia?", Zabibu aliniuliza baada ya kuniangalia kwa muda mfupi.

Nilimweleza yaliyompata Veronika, na jinsi urafiki wetu na Veronika ulivyokuwa umekomaa tangu kuonana mwenye ndege wakati tukielekea Freetown. Hakika nilijuta kumfahamu Veronika afadhali nisingeonana nae.

"Usisikitike sana, sasa tunakuwa watu wawili tuliopoteza marafiki zetu. Lililopo sasa ni sisi kutiana moyo na kusaidiana kuwatafuta hawa waliofanya matendo haya.

Nilijisikia vizuri kidogo Zabibu kuwa pamoja nami.

"Unajua Shuta anapokaa?", niliuliza.

"Ndio, anakaa Oysterbay, Kaunda Drive No. 11230".

"Basi, sasa wewe tulia hapa mimi nitarudi muda si mrefu".

"Twende sote".

"Hapana. Kazi hii huijui niachie mimi, wewe pumzika hapa. Ukiona usingizi chumba hicho hapo kalale. Tutaonana baadaye".

"Lakini jihadhari inaonekana watu hawa ni hatari kabisa, sitapenda kusikia umeuawa, nikisikia tu na mimi nitajiua", aliniambia Zazibu akionyesha hali ya mapenzi kama kwamba tumekuwa marafiki siku nyingi.

Mimi huwa sielewi kwa nini binadamu hawa hutokea kunipenda mara tu nionyeshapo uso wangu. Niliondoka na kuelekea Oysterbay. Niliingia Kaunda Drive na kuanza kuangalia namba za nyumba. Niliendesha polepole mpaka nikaona nyumba. Nilipokuwa napita mbele ya lango la nyumba hiyo mlango wa mbele ulifunguliwa mimi nikaendelea mbele kidogo nikaegesha gari langu, halafu nikarudi kwa miguu.

Nilipofika kwenye ua wa jengo hili nikabana, maana watu wanne walikuwa wanazungumza hapo nje na kulikuwa na magari mawili.

Niliposogea nilisikia mtu mmoja anazungumza.

"Hay Shuta, zungumza na mzee halafu utatukuta Sliver Sands marquuis Du Zaire wanapiga huko mpaka saa kumi. Baada ya kazi ngumi namna hii mtu inambidi astarehe kidogo".

"Sawa Mlambo, ngoja nizungumze na mzee nimpe taarifa yote ilivyo halafu nitampitia msichana wangu na mnamo saa tano hivi nitakuwa huko", alijibu Shuta.

"Oke tutaonana", alijibu Mlambo.

Kisha Mlambo na wenzake wakaingia ndani ya gari aina ya Peugeot 504 na walipotokeza kwenye mlango nikaona namba zao TZ 66500. Shuta alirudi na kuingia nyumbani. Mimi niliruka kama paka nikatua ndani ya ua. Baada ya kutua nikasikia viatu vinatembea kwa nje. nikarudi haraka haraka nikabana ndani ya ua wa michongoma. Nilipoangalia nikaona alikuwa ni askari wa usiku aliyekuwa analinda ile nyumba. Bila kuniona alizunguka kunipita kwenye upande huu wa kulia wa nyumba. Nyumba yenyewe iliwa kushoto mwa barabara kama unatoka mjini.

Alipotangulia tu mimi nilimnyemelea bila yeye kunisikia. Nilipokuwa karibu nae nilimrukia na kumtia kabali, taratibu na bila kupiga kelele nilimnyonga na kuhakikisha amekufa kisha nilimsogeza pembeni kwenye giza la michongoma. Kisha nilizunguka nyumba kuangalia hali ilivyo. Nyumba yenyewe ilikuwa na vyumba vitatu vya kulala. Kulikuwa na chumba kimoja kikubwa nikajua hiki ndicho mwenye nyumba alikuwa akilala. Madirisha yalikuwa yamefungwa. Nikatoa pete yangu yenye jiwe la almasi, nikakata tundu katika kioo kisha nikaingia mkono karibu na mahali pa kufungulia dirisha. Baada ya kufungua dirisha la kioo, kulikuwa na dirisha jingine la wavu wa kuzuia mbu. Nilichukua mkasi nikakata sehemu kiasi cha kupitisha mkono karibu na mahali pa kufungulia nikalifungua.

Nilipanda na kutumbukia ndani ya chumba cha kulala kilichokuwa na bafu ndani yake. Nilifunga madirisha vizuri nikaacha mapazia kama yalivyokuwa yamekunjwa. Nilinyata mpaka kwenye mlango nikasikia mtu anasema kwenye simu.

"Hallo naomba mzee. nimepiga karibu dakika tano nzima sipati namba hiyo. Mimi Shuta hapa.

Nilisubiri pale kwenye mlango wa kutokea sebuleni.

"Hallo, Shuta hapa".

Mambo hayakwenda vizuri sana yule msichana ni mpiganaji wa karate na judo sijawahi kuona. Ameua vijana wetu wanne, watatu aliwaua kabla ya kuchomwa kisu, lakini hata wakati amekwisha kuchomwa kisu alimwua Shilonda kwa kumvunja shingo. Lakini hata hivyo nimemwua.

"Nina uhakika kabisa amekufa palepale maana nilimchoma kisu kwenye moyo hasa".

"Ndio sasa tumebakiza wawili ndipo tunaweza kuanza kupakia".

"Haya asante mzee".

Kisha nilisikia anapiga simu tena. "Hallo Sakina yupo. Shuta hapa".

"Aha kisura jitayarishe nakuja kukupitia twende kamanyola nasikia siku hizi wana mtindo mpya wa 79 Scania LBT III... tutakwenda ukauone".

"Dakika kumi na tano nitakuwa hapo".

"Haya kwaheri".

Akarudisha simu.

Nilijua atakuja chumbani hivyo mimi nilijibanza kwenye ukuta karibu na mlango nikamsubiri maana nilisikia viatu vinakuja. Mkono wa kushoto nilishika bastola na mkono wa kulia kisu kile kilichomwua Veronika.

Alifungua mlango akawasha taa huku akipiga mluzi kisha alifululiza kwenda kwenye kabati la nguo bila hata kuniona. Mimi nilirudisha mlango kwa mguu, ndipo akageuka kuniona. Sijaona mtu anastuka namna hii maana palepale jasho lilimtoka, akataka kukaa chini akashindwa, akaanza kugwaya. Nilifikiri atazirai.

"Kumbe wewe unaona kuuwa wenzako ni rahisi na kumbe wewe mwenyewe unaogopa kifo namna hii".

"Niache niache, mimi ninakujua wewe ni nani, nisamehe".

Kuomba kwake msamaha kulinifanya mimi nikasirike zaidi.

"Kabla sijafikiria kukusamehe nataka kujua kiongozi wenu ni nani?".

"Mimi simjui; mimi ni mtu mdogo tu".

"Si unasema mimi unanijua?".

"Ndiyo nakujua wewe ni Willy Gamba, mpelelezi mkuu wa Afrika. Mimi niliwaambia waaache kama wewe wamekuingiza katika upelelezi lakini walikataa".

"Wakina nani?".

"Akina Mlambo".

"Mlambo ndiye nani?".

"Ndiye mkuu wetu sisi kwa upande wa kuua wapinzani".

"Na yeye ni mwanachama wa SANP?".

Alitoa macho na kushitushwa sana na swali langu hili, kisha nikaona anaanza kutokuwa na mshituko.

"Sitasema maneno zaidi nifanye unavyotaka".

"Ahaa, mimi huwa napenda watu shujaa kama wewe".

Niliweka bastola yangu ndani ya mkoba wake nikaweka kisu vizuri kwenye mkanda nikamfuata. Aliponiona sina silaha akaona ajaribu bahati yake. Palepale aligeuka mbogo na kuanza kunishambulia kwa makonde. Alitupa konde la kwanza nikaliona. Akatupa la pili nikaliona. Akatupa la tatu nikashika mkono wake nikamchukua judo na kumtupa upande mwingine wa chumba akaanguka kama papai bovu. Haraka haraka nikamfuata pale chini nikampiga teke la mbavuni na lingine la tumboni akalainika. Kisha nikamkunja vizuri sana. Nikatoa kisu nikachana shati lake akabaki tumbo wazi.

"Sasa utanieleza. Usiponieleza nitakutumbua matumbo na Sakina hutamwona tena. Niambie nani mkubwa wenu?".

Macho ya kutisha yalimtoka kwa kukiangalia kisu na kuona kuwa nilikuwa sitanii.

"Niache, niache nitakwambia mkubwa wetu ni...

Kabla hajamaliza kusema mlango ulipigwa teke na mtu mmoja akaingia ndani na kabla hajafyatua risasi pale tulipokuwa nilijirusha upande mwingine risasi zake zikanikosa ila zikamwingia Shuta tumboni, na mimi wakati ule ule nikamtupia kisu kilichompata katikati ya koo akaanguka chini huku risasi zinatoka ovyo.

Nilisikia vurumai nyingine sebuleni nikajua wako wengi. Kama umeme nilitoa bastola yangu tayari kukabiliana na matatizo.

"Mashuka umempata?", nilisikia sauti inauliza kwa woga.

"Ndiyo", nilijibu kwa sauti ya chini.

Kabla sijampa nafasi nilijirusha na kujiviringisha ndani ya sebule ambamo nilikuta watu wawili mmoja akiwa na bastola. Na kwa vile hakutegemea hatua kama ile alishikwa na bumbuwazi palepale nikapata nafasi ya kumpiga risasi ya katikati ya paji la uso akaanguka chini. Kabla sijawahi kusimama yule mwingine alipiga teke bastola yangu ikaanguka chini, palepale akanipa teke la tumboni nikaanguka chini. Wakati ule ule nikaona anaangalia kule bastola ya yule mwenzake niliyempiga risasi ilikoangukia na akaruka kuichukua. Mimi nikitumia ujuzi wangu wa miaka mingi nilimwahi wakati ndipo anafikisha vidole vyake kwenye bastola nikampiga kichwa kimoja cha sisimizi akaona nyota na kujiviringisha mbali na bastola. Kwa vile alikuwa tayari amenitia mori nilimfuata wakati naye anasimama. Nikaona anajikunja tayari kupigana karate, mimi nikaona ndipo ananipeleka nyumbani.

"Aisee mlambo-iiiiji mjukuu wa Chaka mwana Zulu fanya kazi yako", alijitia mori.

"Ungekuwa mjukuu wa Chaka ufanye jambo la aibu kama kuwa kibaraka wa Makaburu - tazama Mwafrika asiye na aibu".

Aliruka na kutupa karate nikaikinga kwa mikono. Akatupa tena nami nikaizuia, halafu akageuza mara moja, akanipata, kisha akanipata tena, nikajua huyu alikuwa na ujuzi wa kutosha hivyo mimi ilinibidi nibadili na kujaribu Kung-fu. Na hapo hapo nikasikia mwili mzima unasisimka nikamwingia. Kwa sababu ya hasira na baada ya kukumbuka mauaji ya Veronika chuki kubwa iliniingia hivyo nilitupa wimbi la kwanza nikatupa la pili likampata
la tatu nilipopeleka kiganja changu kikamtoboa chini kidogo ya kifua na kutoka na vipande vya matumbo na vitu vingine vya ndani. Alipiga kelele

"Eeeeeeeeeeeeenakufa, eeeeeeee.

Akaanguka chini akafa.

Nilirudi chumbani nikamkuta Shuta yu hai, anajaribu kusimama lakini anashindwa sababu ya risasi zilizomwingia tumboni. Nilichomoa kisu kutoka kwenye maiti ya yule mtu niliyekuwa nimemchoma kooni nikamfuata.

"Kama ulivyomwua Veronika na mimi nakuua hivyo hivyo, maana nilimwahidi aliponiomba nimlipizie kisasi"

"Nisamehe, nipeleke hospitali".

Kusikia hivi roho ilinichemka, nikamchoma kisu katikati ya moyo huku analia hovyo.

"Kwa heri Shuta, mtaonana sasa hivi na Veronika mbele ya Mungu, ukajibu vizuri kwanini umemwua".

Niligeuka na kumwacha anakufa.

Nilipofika sebuleni tu nikasikia gari linapiga breki pale nje. Niliruka nikachukua bastola yangu na kuokota nyingine hapo sebuleni nikabana karibu na mlango wa kutokea nje nikasubiri.

Mlango ulipigwa teke na hapo hapo wakaingia watu wawili kama risasi, bastola mkononi, wakajiviringisha mmoja akiwa tayari kupambana na kitu chochote mbele yake na mwingine akajiviringisha na kuegeka nyuma. Mimi nilikuwa tayari kwa lolote.

"Ni mimi usiftatue", nilipiga kelele.

Kumbe hawa walikuwa ni Eddy na Sherriff.

Oh Bosi, samahani", Eddy alisema huku akiruka.

"Siku nyingine kutatokea ajali namna hii", nilimwambia.

"Tunaomba isitokee", Sherriff alijibu naye akisimama.

"Umefanya kazi kubwa sana Bosi", Eddy alinipongeza baada ya wao kuangalia maiti zote ndani ya nyumba hii.

"Ninastahili kazi kama hii", nilijibu.

"Sisi tulipongojea kwa muda mrefu tukaona tukufuate baada ya kujua kutoka kwa Zabibu kuwa umekuja huku. Tulihisi kuwa kuchelewa kwako unaweza ukawa katika matatizo. Tulipokuja tulikuta gari lako na gari jingine hapo mbele yameegeshwa. gari lako lilikuwa limetolewa upepo ndani ya tairi zote, hivyo hii ilituhakikishia kuwa uko msambweni", alieleza Eddy huku tukielekea kwenye gari lao. Ndani ya gari nilimkuta Zabibu.

"Oh Willy mpenzi uko salama?".

Alifungua mlango na kunirukia akiweka mikono shingoni mwangu na kunibusu.

"Na wewe umefuata nini?", nilimwuliza.

Nilimkarisha ndani ya gari kwenye viti vya nyuma mimi nikakaa huku Sherriff na Eddy wakaingia mbele, Eddy akatia gari gea tukaondoka.

"Nilikuja nikuone kama ni kufa tufe wote. Maana sijui nini kimeniingia nakuona wewe ndiye mwenzangu sasa. Nikiwa karibu na wewe nasahau yote yaliyopita".

"Usizoee kutembea na sisi mtoto kama wewe, hufai hata kujeruhiwa kidogo. tuachie sisi hatari ndiyo kazi yetu. Sitaki kupatwa mkasa kama niliopatwa nao kwa Veronika".

Kisha nikamweleza toka mwanzo mpaka mwisho wa mapambano yangu nyumbani kwa Shuta.

"Naona huyu Mlambo na wenzake walitia shaka walipoona gari langu. Hivyo walirudi kuhakikisha. Lazima niseme Mlambo alikuwa na mafunzo ya hali ya juu ya jeshi hata mimi alinitoa jasho".

Tulielekea nyumbani kwa Eddy.

ITAENDELEA