Saturday, March 9, 2013

NJAMA


SURA YA TISA

MAPAMBANO NA VIBARAKA

Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu za asubuhi wakati nilipokuwa nakaribia kumaliza kunyoa ndevu. Nilikiangakia kidevu changu kwenye kioo nikaona nilikuwa sijajinyoa vizuri. Kila wakati nilipokuwa na mawazo mengi kitu kama hiki kilikuwa kinanitokea . Lakini hata hivyo nia yangu nionekane nadhifu hivyo nilichukua tena mashine ya ndevu na kuanza kujinyoa. Nilipoona mambo yanakuwa mazuri kwenye kidevu changu, nikaanza kuoga.

Nilitoka maliwatoni na kurudi chumbani nilikokuwa nimelala. Zabibu bado alikuwa hajaamka, hivyo nilivaa taratibu ili nisije nikamshtua toka usingizini. Alikuwa na sura ya mtoto mchanga isiyokuwa na maneno. Nilimwangalia huku nikivaa. Nilipomaliza kuvaa na kuweka kila kitu changu tayari, nilikwenda nikambusu Zabibu usingizini nikaondoka ndani ya chumba na kufunga mlango taratibu.

Niliwakuta Sherriff na Eddy wamekaa sebuleni wanakunywa kahawa.

"Karibu bosi, habari za kuamka?".

"Nzuri", nilijibu, nikaa kwenye kiti cha meza ya kulia nikavuta kikombe cha chai na kujiwekea kahawa ya kutosha.

"Lazima iwe nzuri", Sherriff alijibu huku akitabasamu nikajua alikuwa na maana gani kusema hivyo.

"Usinionee wivu".

"Lazima tukuonee wivu, maana chuma kama hicho si cha kawaida.

"Bosi, vijana wameleta habari kama ulivyoomba", Eddy alisema huku akibadilisha mazungumzo.

"Ndio, wamesemaje.

"Wamesema hawakuweza kumwona Sikazwe mpaka saa tisa za usiku. Walimpata akitokea kwenye barabara ya Bagamaoyo na akielekea nyumbani kwake. Hawakuweza kujua alikuwa anatokea wapi. Na mpaka sasa hivi bado yuko nyumbani amelala. Wamenieleza kuwa ofisi za SANP hazifanyi kazi siku za Jumamosi. Na kama unavyojua leo ni Jumamosi".

"Basi waambie waendelee na wahakikishe kuwa hawapotezi hata dakika moja. Atakapoondoka nyumbani nataka kujua anaelekea wapi. Sawa?".

"Hamna taabu".

"Sasa hivi mimi ninakwenda kumwona Chifu maana nilipata habari kuwa anataka ripoti toka kwangu, maana anasumbuliwa sana na Serikali".

"Nafikiri Sherriff anaweza kuendelea kupumzika hapa, mimi nitakujulisha wakati nitakapokuhitaji".

"Sawa", alijibu Sherriff kwa mkato.

"Naomba unipatie 'machine gun' inayoweza kuchukua risasi zaidi ya mia. Niliwahi kuzitumia nilipokuwa jeshini.

"Aina gani".

"Zilizotengenezwa Urusi".

"Zipo".

"Oke niletee moja ya aina hiyo. Ikiwezekana tuma mtu aniletee mapema kusudi niishughulikie".

"Hamna taabu, utapata.

Baada ya kuzungumza na hawa vijana tuliagana kisha nikaondoka. Nilitembea kwa mguu mpaka nyumbani kwangu, ili nikabadilishe nguo. Nilifika nikafungua mlango, nikaangalia saa yangu nikaona ilikuwa yapata saa mbili kasoro robo. Nilipoingia tu ndani, roho yangu ikashtuka lakini nilikuwa nimechelewa, nilipigwa na mfuko wa mchanga kisogoni nikaanguka.

II

Nilisikia sauti ikisema ni saa tisa sasa. Sauti hiyo ndiyo ilikuwa imenizindua. Nilijikuta nimelazwa kwenye kitanda cha chuma bila godoro, na nilijikuta nimefungwa kwenye kitanda mikono na miguu. Kichwa kilikuwa kinaniuma sana, na kwa chati nilifunua nilikuta nimo kwenye chumba kidogo cha giza tupu.

Nikatuliza mawazo nikaanza kufikiri nini kimetokea. Ndipo nikatambua kuwa nilipokuwa nakwenda nyumbani kwangu saa mbili kasorobo nilipigwa na kitu nilichohisi ni mfuko wa mchanga nikaanguka chini. Tokea hapo mpaka sasa sikujua chochote. Hii ina maana kuwa nilizimia. Nikakumbuka yule mtu alisema ilikuwa saa tisa, hii ina maana nilikuwa nimezimia kwa zaidi ya masaa sita.

Nilifikiri jinsi akina Eddy, Sherriff, zabibu na Chifu walivyokuwa wamehangaika huu kujaribu kunitafuta. Hata mimi mwenyewe nilikuwa sijui hapa ni wapi. Ila nilikuwa nasikia kelele nyingi nje ya chumba hiki. Hivyo nilifikiri kuwa huenda ikawa ni sehemu ya viwanda. Sikujua ile sauti iliyosema sasa ni saa tisa ilitokea wapi, maana kulionekana kana kwamba hakukuwa na mtu ndani ya chumba hiki.

"Zaidi ya saa tisa sasa lazima waje kutupokea sisi twende tukapate chochote", nilisikia tena mtu anazungumza.

"Washa taa", sauti nyingine ikajibu.

Hivyo nikajua kuwa nilikuwa nalindwa na watu wawili ila sikuweza kuwaona kwa sababu ya giza. Taa ilipowashwa mimi nikajifanya kana kwamba bado nimezimia kabisa.

"Bado kazimia kabisa", alisema mmoja wao.

"Daktari alisema hawezi kuamka mpaka saa kumi na mbili au baada ya hapo", alijibu mwingine.

"Kama ni hivyo basi twende tukawaambie watupokee njaa inauma sana".

"Oke twende, zima taa".

Walifungua mlango na kuzima taa halafu wakafunga mlango na funguo wakaondoka. Mimi nilijinyanyua ili nione nimefungwa kiasi gani. Nilikuta ni mikono na miguu tu iliyofungwa kwenye kitanda cha chuma kipatacho futi tatu upana. Miguu ilifungwa kwa ustadi sana kiasi kuwa nilisikia kama damu haipiti na sehemu za nyayo zimekufa ganzi. Kwa upande wa mikono, mkono wa upande wa ukutani nilipoujaribu nikaona haukufungwa kwa ustadi sana, ule wa upande mwingine ndio ulifungwa kwa ustadi sana.

Nilinyanyua kichwa changu nikasikia kinauma sana, nikakirudisha chini. nilianza kufikiri namna gani nitajiokoa. Baada ya kufikiri sana nikaona njia pekee ni kujaribu kufungua hizi kamba kabla walinzi hawa hawajarudi. Hivyo nilionelea nijikaze. Ingawaje kichwani nilisikia maumivu makali. Kwa vile sehemu zote tokea tumbo, kifua na kichwa zilikuwa hazikufungwa, na kitanda kilikuwa cha futi tatu nilijikunja ili mdomo wangu ufikie kamba za mkono wa upande wa ukutani ambao haukuwa umefungwa sana.

Nilitulia tena nikamwomba Mungu. Niliupeleka mdomo wangu kwenye fundo la kamba walilokuwa wamenifungia. Kwa bahati mdomo wangu ulifika nikaanza kupitisha meno yangu kwenye kamba ili niweze kujua wamefungaje. Katika hii tafuta tafuta huku maumivu karibu yananitoa fahamu, niliuma ncha moja ya kamba, nikaivuta na fundo lote la kamba likafunguka na mkono wangu wa kulia ukawa huru.

Ilibidi nirudishe kichwa changu kipumzike maana maumivu yangu yangeweza kunifanya nizimie.

Nikiwa na mkono mmoja huru, nilipata tumaini na nguvu mpya. Nilichoomba sasa ni watu hawa wasije upesi. Kwa vile walikuwa wamesema daktari aliwaambia siwezi kuamka kabla ya saa kumi na mbili nilijua watadharau kuja ndani ya chumba hiki cha joto la kuweza kuua kabla haijakaribia saa kumi na mbili wakati wananitegemea kuamka. Nguvu mpya zilizoletwa na mawazo kuwa nimechelewa mambo mengi zilinifanya nisahau kabisa maumivu yangu.

Niliutumia mkono wangu wa kulia kufungua mkono wa kushoto. Nikiwa sasa nimeweza kufikia hatua hii niliingiwa na furaha nikaanza kushambulia kamba nilizofungwa miguuni. Kwa mtu mwenye ujuzi kama wangu hii haikunipa taabu na mara nikawa huru tayari kupambana na wadhalimu hawa.

Nilirudi nikajilaza nikaziweka kamba kijanja kana kwamba bado hazijafunguliwa. Nikawa katika hali ya kusubiri. Nilivyokuwa na bahati haikupita muda mrefu nikasikia funguo zinaingia ndani ya kufuri la mlango. Mara mlango ukafunguliwa na taa zikawashwa. Mimi nilijilaza vile vile na kujifanya bado nimezirai.

"Bado sana huyu, niliwaambia daktari alisema saa kumi na mbili. Angekuwa mtu wa hivi hivi asiye na mazoezi pigo lile lingemuua pale pale", nilisikia sauti ikisema.

"Sawa. Akiamka saa kumi na mbili itakuwa vizuri maana ndipo wakati wazee watakapomhitaji", sauti nyingine ilijibu.

"Haya shika funguo, mwangalie kwa makini akionyesha dalili ya kupata fahamu tupashe habari mara moja. Sisi tuko chumba kingine tukisubiri maelekezo zaidi kutoka kwa wazee.

"Haya asante, lakini naomba asiamke wakati nikiwa peke yangu. Nasikia mtu huyu ni hatari kubwa kabisa'.

"Wewe mwoga sana. Mtu aliyefungwa kiasi hiki unafikiri atafanya nini hata akiamka, labda awe na nguvu za kishetani".

"Huenda anazo".

"Kama anazo basi pole, yatakuwa matatizo yako".

Nikiwa katika kusikiliza mazungumza haya kidogo nicheke. Yule mtu mwingine alitoka, akabaki mlinzi mmoja ambaye alifunga mlango na kuzima taa, halafu akakaa kwenye kiti. Nilisubiri kama dakika kumi hivi nikaanza kukoroma. Yule mlinzi aliinuka na kuwasha taa na kunisogelea kitandani wakati mimi bado nimefumba mamcho. Kule kuhema kwake ndiko kulinifanya nijue yuko karibu.

"Wewe umeamka", aliuliza kwa wasiwasi, nilifungua macho yangu kwa chati nikaona alikuwa ameshika bastola akiwa amelenga kifuani pangu. Nilifanya mahesabu ya namna ya kumwingia mtu huyu nikapata.

"Ndiyo', nilijibu kwa unyonge.

Niliona macho yanamtoka, nikaona mtu huyu ameingiwa na woga na anaweza kunipiga risasi shauri ya woga nisipomwahi. Hivyo kama chui nilimrukia na wakati ule ule nikawa nimepiga bastola yake ikaanguka upande mwingine na nikampiga pigo la mkono la karate katikati ya kichwa akafa bila kujua nini kimemwua. Niliiendea bastola yake, nikamvua joho lake jekundu, nikalivaa, kisha nilifungua bastola nikakuta funguo na risasi za bastola hii. Nilifungua bastola nikakuta ina risasi tatu tu nayo ina uwezo wa kubeba kumi. Hivyo niliijaza risasi, kisha nikachemsha kidogo viungo vyangu tayari kwa kupambana na watu walioko chumba kingine. Kichwa kilikuwa bado kinaniuma lakini hakikuwa tishio kubwa.

Nilizima taa, nikajaribu kufikiri nilipo lakini nikaona bila kwenda nje haingenisaidia. chumba hiki kilionekana kilikuwa ni stoo ya vitu, hivyo nilihisi hapo nje kuna ofisi na nilifikiri kuwa ndicho chumba cha pili alichokuwa amezungjumzia yule mlinzi wa pili. Nilifungua mlango taratibu, niliangalia hali mara moja nikajua hizi zilikuwa sehemu za nyuma za bohari, au ofisi. Maana kulikuwa na chumba kinatazamana na stoo hii, halafu kulikuwa na vyumba vitatu mbele tena kwa upande wa kulia. Upande wa kushoto kulikuwa na mlango wa kutokea uwani.

Nilisikia watu wanazungumza kwenye chumba kilichokuwa kinaangaliana na mahabusu yangu. Nikajua ni hiki chumba alichozungumza yule mlinzi. Nilijiweka tayari kisha nikagonga. Mimi niliamini watajua ni mwenzao hivyo wangekuja bila tahadari kufungua mlango.

"Ngwishe", nilisikia sauti ikiita.

"Ndiyo", nilijibu kwa sauti nzito.

"Ameamka?".

"Bado".

"Funguo tu mlango haukufungwa", nilijibiwa.

Basi bastola yangu ikiwa tayari mkononi, nilifungua mlango na kuingia ndani. Kweli watu wote sita walikuwa wamwezunguka meza wanakula. Waliponiangalia na kunitambua mimi ni nani wengine chakula kiliwadondoka toka midomoni.

"Endeleeni kula, mbona mnaacha", niliwatania.

Mmoja wao alimkonyeza mwenziwe wakifikiri mimi sikuona kumbe hawakujua macho ya Willy yamefundishwa kuangalia kila mahali kwa wakati mmoja utafikiri kinyonga. Yule aliyekonyezwa alitoa bastola haraka sana lakini mimi nilijua anataka kufanya nini na kabla hata sijamtahadhalisha alikuwa tayari kufyatua, lakini mimi nilikuwa mwepesi zaidi nikampata. Wakati yeye alipofyatua risasi alimpiga mwenzake na kumwua. wawili tayari walikuwa wamekufa.

Pale pale wengine wote walisimama kila mtu akitoa bastola. Lakini niliwawahi watatu halafu nikaona yule wa nne macho yake yanaangalia mlango. Mara moja nikaanguka chini na risasi ikanikosa kwa nyuma ikapita na kumpiga yule wa nne na kummaliza, mimi pale pale nikajiviringisha na kumwahi yule wa nje. Lo nilikuwa nimeponea chupu chupu, maana kama nisingewahi kulala chini, vile vile ningekwenda kuonana na Veronika mpenzi wangu kama kweli watu huwa wanaonana tena huko ahera.

Nilitoka ndani ya jengo hili upesi upesi. Nilipofika nje nikaona niko kwenye mabohari ya Chang'ombe. Bohari hii ilikuwa imezungukwa na ua wa matofali. Nilivua joho jekundu nikapanda ua nikatokea katika uchochoro nikaanza kukimbia. Nilikadilia kuwa ilikuwa yapata saa kumi na moja. Nilipofika mbele ya bohari nilikuta ni mali ya Kampuni moja ya matairi ya magari iitwayo "Trans World Tyres", kwa sababu sikutaka kufanya uchunguzi zaidi kutokana na hali niliyokuwemo niliona teksi nikaipungia ikasimama na kumwamuru dereva anipeleke Independence Avenue haraka.

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment