Saturday, March 9, 2013

NJAMA


SURA YA NANE

BINTI TANZANIA

III

Tulipofika nyumbani kwa Eddy ilikuwa saa tano za usiku. Tuliingia tukaa kwenye viti. Eddy akaleta vinywaji.

"Kifo cha Veronika kimeniuma sana, tokea sasa mimi nimeahidi nitakuwa bega kwa bega na wewe mpaka nione mwisho wa mambo haya", Sherriff aliniambia huku machozi yakimtoka.

"Sijui nikwambie nini Sherriff, maana hali niliyonayo mimi siwezi kuieleza. Afadhali tuiachie hapo hapo".

"Basi, mambo yote tumetengeneza. Chifu amesema mwili wa Veronika hauwezi kusafirishwa mpaka mwisho wa mambo yote ili aweze kupewa heshima zote za kijeshi. Hivyo mwili wake umetunzwa huko kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya Muhimbili mpaka hapo tutakapojua mwisho wa mambo haya. Mwili wake utapewa uangalizi wa pekee hivyo hata tukichukua mwezi mzima utakuwa katika hali safi tu", Eddy alieleza.

"Jambo hili haliwezi kuchukua siku mbili zaidi. Nimeshapata mwanga mkubwa wa kutosha. Kuna kitu kidogo tu ambacho bado kinakosekana lakini naamini kesho haiishi bila kukupata kitu hicho", niliwaeleza. Kisha nikawaeleza jinsi nilivyokuwa ninafikiria mambo yalivyo toka mwanzo mpaka mwisho.

"Sasa ninachotafuta ni yale magari waliyapata wapi?.Nguo ni rahisi pamoja na vyeo kama nilivyowaeleza. nikishajua hilo basi jambo hili tutakuwa tumelitatua. Itabaki sasa kufanya shughuli ya mwisho ambayo ni kuzikamata hizi silaha na kuwakamata vibaraka hawa".

Wote walitingisha vichwa kuonyesha wamenielewa.

"Ray Sikazwe anakaa wapi?", nilimwuliza Zabibu.

"Anakaa Oysterbay, Kenyata Drive nyumba Nambari 1000/D.

"Oke, Eddy tokea sasa hivi weka vijana wa kumfuata Ray Sikazwe kila mahali anapokwenda. Ifikapo asubuhi nataka nataka nijue nyendo zake zote na sisi tutawasaidia tokea hapo. Tukiweza kufanya hivyo kazi itakuwa rahisi. Baada ya mambo yote yaliyotokea leo lazima akipata habari atakuwa na wasiwasi, hivyo lazima tu atafanya kitu cha kujinasa. Wote tutalala hapa maana ndiko mahali hapafahamiki.

"Tutaonana asubuhi", niliwaaga.

Nyumba ya Eddy ilikuwa na vyumba vitatu vya kulala. Kwa vile Zabibu alikuwa na huzuni nyingi na kwa vile mimi pia nilikuwa na huzuni tulionelea afadhali tukalala pamoja ili tuweze kuliwazana mioyo.

ITAENDELEA

1 comment:

  1. Baccarat - Live! Casino
    Baccarat has become the leading table game 인카지노 of all time. Bet in this game in the popular 4th of July, the bet will 바카라 be placed febcasino on a banker's side.

    ReplyDelete