Saturday, July 9, 2011

Siku ya siku imetia

Pambano la watani wa jadi Yanga na Simba
Makocha Presha juu

Na Nyakasagani Masenza
Makocha wawili raia wa Uganda Sam Timbe wa Yanga na Basena wa Simba, timu ambazo ni mahasimu wakubwa kutambiana kwa muda mrefu, siku yao imetimia zitakapokuta leo kwenye mchezo wa fainali ya Kagame Castle Cup, utakaochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam majira ya saa 10 Alasiri.

Yanga walitinga fainali kwa njia ya matuta ya penati na kuiondosha St. George ya Ethiopia, kama ilivyo kwa Simba nayo ilitinga katika hatua hiyo kwa matuta dhidi ya El Merreikh ya Sudan.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya pili baada ya miaka 19, katika hatua ya fainali za Kagame Castle Cup, ambayo awali ilijulikana kama Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.

Mwaka 1992 zilitinga katika hatua hiyo na kukipiga kwenye Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar, kuanzia majira ya saa mbili usiku, ambapo Simba walitwaa Kombe hilo kwa mikwaju ya penati, baada ya winga hatari wa Yanga wakati huo Abubakary Salim kukosa penati ya mwisho.

Hata baada ya mwamuzi wa mchezo huo Nasoro Hamudani kutoka Kigoma kuongeza penati moja moja kila upande, beki wa kutumainiwa wa Yanga wakati huo David Mwakalebale, alipiga mpira nje na kuifanya Simba kutwaa Kombe hilo kupitia kwa mshambuliaji wake wakati huo Issa Kihange.

Mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, hususan baada ya makocha wa timu zote kufanya usajili, Yanga inatarajiwa kuwatumia washambuliaji wake Jerryson Tegete, ambaye mara kadhaa amekuwa akimtungua kipa namba moja wa Simba Juma Kaseja. Tegete atashirikiana na Davis Mwape na Keneth Asamoh.

Kwa upende wa Simba, Mussa Hassan Mgosi ambaye mara kadhaa amekuwa akisababisha rabsha langoni mwa Yanga, anatarajiwa kuonesha cheche zake, akisaidiwa na Ulimboka Mwakingwe na Haruna Moshi Boban.










 

 

No comments:

Post a Comment