SURA YA KUMI
"UHURU UTALETWA KWA MTUTU TU"
III
Tulitoka kwenye kichochoro kimoja kati ya mabohari ya sehemu hii na kujikuta uso kwa uso na bohari ya intercontinental Motors. Tulikuta nje kuna malori matatu yanapakiwa kwa pamoja. Kulikuwa na watu wasiopungua ishirini, walikuwa wanapakia mizigo kwa kupeana. Tuliona gari la Sikazwe lakini yeye hakuwemo, hali hii ilitujulisha kuwa yumo ndani.
Penbeni kidogo ya magari haya kulikuwa na walinzi. Walikuwa hatua kama ishirini kutoka kwenye magari yaliyokuwa yanapakia kwa kila upande; baadhi yao walikuwa wamejibanza kwenye ukuta wa mabohari haya na mengine wote wakiwa na bunduki mkononi. Habari nzuri wote walivaa majoho mekundu na kofia. Nilihisi kuwa kulikuwa na askari wasiopungua ishirini hapa nje.
"Nafikiri wote mmeona ulinzi ulivyo. Kitu ninachotaka ni kufanya mashambulizi kimya kwanza mpaka tutakapolazimika kuwashambuliwa watu wa ndani. Kwa upande huu giza linatusaidia hivyo walinzi wa huku haitakuwa taabu kuwapata. kuna walinzi kama sita waliobana upande huu. Mimi na Isaack tutashambulia kushoto, Nyinyi Sherriff na Eddy mtashambulia upande wa kulia. Nawatakia kheri".
Tulipeana mikono kimya kimya kwani hatukujua nini kitatokea. Mimi nilikuwa wa kwanza kujitokeza kwenye michongoma na kubana kwenye huu ukuta wa bohari jingine. Kama hatua tatu kulikuwa na mlinzi anavuta sigara huku macho yake yakiwa kwenye gari. Nilimsogelea kimya kimya. Nilipokuwa karibu kabisa nilimsemesha.
"Sijui watamaliza saa ngapi kupakia, mimi najisikia kuchoka".
"Sijui hata..." Aligeuza uso kunijibu, nikamkata karate ya shingo upesi upesi na kumlaza chini. Nikamwashiria Isaack alipojitokeza nikamwona Eddy naye ananyata kwenda upande wa kulia. Nilimnyooshea kidole kimoja kumweleza mmoja tayari nimepata. Yeye akanitolea alama ya vidole ya V kuonyesha ushindi.
"Wewe Isaack simama hapa hapa uwe kama wewe ndiye mlinzi wa hapa, mpaka nitakapokuonyesha ishara nyingine".
"Sawa", alijibu.
Mlinzi mwingine alikuwa hatua kumi hivi na hakujua nini kimetokea. Kwa vile nilikuwa nimevaa kama yeye alifikiri mimi ni mwenzake hivyo nilikwenda tu kama mmoja wao mpaka nilipomfikia.
"Vipi kuna wasiwasi wote?", nilimwuliza.
Aliinua kichwa.
"Hakuna....."
Kabla hajamaliza nilimkata karate ya katikati ya kichwa akafa palepale. Nilimwegemeza vizuri kwenye ukuta nikamwacha kama mtu aliye hai.
Nilimwunulia Isaack vidole viwili na yeye akawainulia Eddy na Sherriff ambao sasa nilikuwa siwaoni. Kumbe Eddy na Sherriff walikuwa wameenda kwa haraka zaidi, maana Isaack alinionyesha vidole vitatu kuonyesha wenzetu tayari walikuwa wameua watatu.
Hii ilinitia moyo sana. Upakiaji uliendelea bila wasiwasi. Mtu wa mwisho kwa upande huu alikuwa amebana kwenye kona kabisa ya ukuta wa bohari hii. Nilimwendea huku nikiwasha sigara. Na yeye alipoiona aliweka bunduki yake chini akatoa sigara.
"Sina moto afadhali umepita huku", aliniambia.
Mimi niliwasha kiberiti akaimana ili kuwasha sigara. Palepale nikamkata karate ya shingo. Bila hata kukoroma akakata roho. Nikamwegemeza ukutani halafu nikamfanyia ishara Isaack aje.
"Sawa wewe utasimama hapa mimi nawafuata walinzi wale watatu waliosimama mbele ya magari. Kama watashtuka mimi nitajitupa chini wewe wawahi". Halafu nikatoa funguo za gari.
"Pita hapa kichochoroni panda gari mpaka ofisini mwambie Chifu aje pamoja na Mkuu wa Polisi pamoja na askari watakaokuja kulinda na kuzihifadhi zana hizi baada ya mapambano. Umenielewa?".
"Sana. Nakutakia kheri".
Nilianza kutembea kuelekea kwa wale watu. Kabla hata sijafika nilisikia mlio wa 'SMG' kwa upande wa akina Sherriff. Nikajua mambo yameiva. Nikainua SMG yangu na kuwateketeza hawa walinzi waliokuwa mbele ya magari. Isaack hakupata hata muda wa kupiga risasi ila nilimwona anaingia uchochoroni na kupotea. Mimi niliruka juu ya gari lililokuwa karibu, nikakuta watu wanne walikuwa wanapanga masanduki ya silaha.
"Kumetokea nini?", niliwauliza.
Wote waligeuka na kuniangalia. Pale pale nikawaachia risasi za kuwaua kisha nikaruka chini. Milio ya bunduki ilifanya watu wote watoke ndani ya bohari na kusambaratika hovyo. Watu wote waliokuwa hapa juu walikuwa wamesharuka chini. Niliweka sanduku moja kama kinga nikaanza kutungua mtu mmoja mmoja na bastola yangu nyenye sailensa.
Kwa vile hawakusikia mlio kutoka sehemu yangu watu walipiga risasi zao kuelekea upande kwa upande wa akina Sherriff. Nilipoangalia juu ya lile gari jingine nilimwona sherriff ameseimama juu na kuwashambulia adui kwa namna ya ajabu.
Nilimfanyia ishara akaiona na yeye akanifanyia ishara ya kuonyesha kuwa Eddy alikuwa chini anajaribu kuingia ndani. Kuona hivyo nilimfanyia ishara kuwa na mimi nakwenda ndani hivyo atuchunge wote. Tulikuwa tumeuwa idadi kubwa ya askari waliokuwa wamebaki ni wachache tu.
Niliruka chini huku nikiachia risasi ovyo hata niliweza kufika kwenye ukuta wa bohari lao. Nilitupa SMG nikajitupa kwenye mlango na kujiviringisha mpaka ndani ya bohari na kama umeme nikarukia nyuma ya sanduku kubwa na kuanza kujaza risasi bastola yangu. Huko nje nilisikia bado Sherriff anaendelea kumimina risasi ili kuwazuia wasitoke nje.
Nilipoinuka niliona kama kumebaki watu kumi tu ndani; wengine wote tulikuwa tumewateketeza. Nilimwona Eddy anaviringisha na kuingia ndani. Wale watu walimwona na kabla hawajapiga risasi niliwahi wawili, wengine wote wakarudi kujificha nyuma ya masanduku.
Eddy aliruka mpaka nilipokuwa.
"Asante bosi umeniponya",
"Usinishukru ndio sababu tuko wote. Kwanza kazi mliyoifanya wewe na Sherriff sikuitegemea. Kazi imekuwa rahis kabisa".
"Kuna watu kama wangapi humu ndani?".
"Hawazidi kumi, na wote wako upande wa mashariki. Nafikiri wanamlinda Sikazwe na Max".
Huko nje kulikuwa kimya; Tukajua Sherriff anasubiri sasa kashi kashi kutoka kwetu.
"Sasa Eddy lazima tuwafanyie ujanja ili tuwapunguze. Mimi nitasimama juu ya hili sanduku ili niwadanganye. Walivyo wajinga walinzi wao watainuka ili wanipige risasi. Mimi nikiita tu jina kaa tayari na hii SMG yako kisha anza kumimina risasi. Mimi nitakuwa nimeisharuka kitambo, hivyo utawapata kama mchezo. Usiogopea kuwa unaweza kuniumiza ninakuhakikishia kuwa nitakuwa sipo".
"Lolote usemalo bosi", Eddy alijibu huku anatayarisha bunduki yake.
Niliinuka kama umeme juu ya sanduku nikawaona wote mara moja.
Nikaita
"Sikazwe?".
Hapo hapo kama umeme nikaruka nyuma ya sanduku jingine. Walinzi wanne wainuka ili kunitupia risasi huku wakiwa wamejitokeza hadi vifua. Eddy alimimina risasi na kuwashindilia wote risasi katikati ya vifua vyao wakafa pale pale. Nilimwonyesha Eddy vidole kuwa wamebaki watatu, kwani nilipokuwa nimeruka juu ya sanduku niliona wako watu saba.
"Gamba, nilisikia sauti ya Sikazwe anaita.
"Unasemaje?", nilimwuliza.
"Naomba tuzungumze, vita umeshinda.
"Sawa Sikazwe, lazima ujuwe kuwa ukombozi wa Afrika Kusini utaletwa kwa mtutu wa bunduki tu, si mazungumzo.
"Walinidanganya".
"Hawakukudanganya, shida yako ni kwamba wewe ni kibaraka; yaani unapenda cheo kuliko watu wako. Matokeo yake ndiyo haya. Hata Makaburu wafanye njama za namna gani, mwisho wake wazalendo watashinda.
Wakati tukijibishana na Sikazwe, Eddy alikuwa anatambaa chini kuelekea pale walipokuwa.
"Tafadhali tuzungumze?", aliomba.
"Umechelewa, maana umeshaipaka matope Afrika, hivyo tutakupeleka mbele ya wanamapinduzi wa Afrika ndio watakao kuhukumu".
"Huwezi kunichukua hai".
Kumbe wakati huu tunajibishana Max naye na askari mwingine walikuwa wamejivuta karibu kabisa na mimi. Ghafla nikahisi kuna kitu karibu nami.
"Bosi", Eddy aliita ambaye pia alikuwa amewaona.
Kusikia tu hivyo niliruka pale nilipokuwa na wakati huo nikawaona Max na yule kijana mwingine karibu kabisa na mimi wameinua bastola tayari kufyatua. Nilijiviringisha hewani namna ambayo hata wao walishangaa risasi zao zote zikanikosa, wakati ule ule nikaachia za kwangu nikawapata wote nao wakaanguka chini.
Sikazwe aliinuka akasimama juu ya sanduku akachukua bastola akataka kujipiga risasi. Bastola tatu zililia kwa wakati mmoja na kuupiga mkono wake. Kumbe Sherriff nae alikuwa amefika mlangoni na kuona kitendo alichotaka kukifanya akakizuia. Eddy nae aliona akazuia wakati na mimi niliona nikazuia asijipige risasi.
"Bado tunakutaka Sikazwe ukiwa hai ili ukajibu maswali ya wanamapinduzi na wapenda maendeleo ya Afrika", nilimwambia huku bado anashangaa jinsi risasi tatu zikitoka pande tofauti zilivyoweza kupiga kiganja chake tu.
Mara tunasikia usiku mzima umejaa kelele za milio ya magari ya polisi.
"Chifu yuko njiani", niliwaambia wenzangu ambao sasa tulikuwa tumemzunguka Sikazwe.
Lo, Bosi ile jiviringisha uliyotoa pale hewani sijaona hata ndani ya sinema", Eddy alinisifu.
"Mimi nilichoka kabisa; sasa naamini yote niliyoelewa. Nilifikiri mengine wanakuongezea", Sherriff alisema.
"Kuwa komandoo siyo mchezo", niliwajibu nikatabasamu.
Milio wa tahadhali ya magari ya polisi ulisogea kabisa.
"Ndio sababu sikumwona Isaack", Eddy alisema.
"Ndio sababu", nilijibu.
Tulisikia milango ya magari inafungwa kwa nguvu. Mara tukamwona Chifu na Mkuu wa Polisi wanaingia.
"Karibu Chifu, kazi imekwisha. Na mtu wenu huyu hapa na mwingine nafikiri tayari una habari naye. Ndani ya malori hapo nje kumejaa silaha, na zingine zimo humu. Mkienda bandari ndogo (dhow wharf) mtakuta meli ndogo iliyotayarishwa kwa ajili ya kusafirisha silaha hizi, sisi hatuna zaidi", nilimweleza kwa niaba ya wenzangu.
"Kazi nzuri vijana, mmeokoa jina la Tanzania, na mmeitoa Afrika katika aibu", Chifu alijibu huku wakitupa mikono ya pongezi.
Mkuu wa polisi alitoa pingu akamfunga Sikazwe huku sura yake ikionyesha ukali.
Mara nikamwona Zabibu anakuja anakimbia akifuatiwa nyuma na Isaack. Niliwakonyeza Sherriff na Eddy, tukatoka pale haraka haraka tukawaacha Chifu na wenzake wanamshughulikia Sikazwe.
"Oh mpenzi Willy", Zabibu alinirukia shingoni.
"Hamna taabu wote tu wazima", nilimjibu.
"Ashukuriwe Mungu", Zabibu alijibu.
"Isaack gari liko wapi?".
"Oh Bosi, linakusubiri wewe".
"Twendeni zetu, acheni wazee hao wafanye shughuli zao sisi yetu tumemaliza", niliwaeleza wenzangu.
Sherriff, Eddy, Isaack, Zabibu na mimi tuliondoka na kwenda kwenye gari letu huku askari polisi tuliowapita wakitushangaa na kutupigia saluti. Tuliingia ndani ya gari letu, huku gari moja la polisi lenye mlio wa tahadhali limetutangulia.
"Je unajua tunakwenda wapi?", aliuliza.
"Sijui lakini nafikiri imebidi tupewe heshima ya 'VIP' Isaack alijubu.
Mara gari nyingine ya polisi ikatusindikiza kwa nyuma.
"Lo, utafikiri Marais", Sherriff alitania.
"Mara moja kwa miaka si mbaya", nilijibu.
"Mimi mnitelemshe kwa Margaret", Sherriff alisema.
"Ala, mipango imeshafanywa nini?", niliuliza.
"Oh, mwenzangu siku nyingi", Eddy alijibu.
"Sawa baba, kazi na dawa", nilijibu huku nikimbusu Zabibu.
Nilipoangalia saa yangu nikaona ilikuwa yapata saa sita kasoro robo.
Ilikuwa asubuhi ya Jumapili. Jua lilichomoza kutokea baharini huku miali yake ya asubuhi ikichukua rangi ya maji ya bahari na kuipitisha kwenye vioo vya chumba changu cha kulala. Mwanga huu ulimmulika Zabibu usoni ambaye alikuwa bado amelala. Hakika mwanga huu wa asubuhi ulimfanya azidi kupendeza. Asubuhi vile vile kulikuwa na upepo baridi uliotoka baharini na kutufikia sehemu hizi za Upanga. Kwa kifupi ilikuwa asubuhi njema ambayo sitaisahau.
Niliangalia saa yangu nikaona inapata saa moja kasoro dakika tatu. Nilinyanyuka na kufungua radio ili kusikia taarifa ya habari ya saa moja. Kunyanyuka kwangu kulimwamusha Zabibu ambaye alinitolea tabasamu la kukata na shoka. Na mimi nikamrudishia lile la pekee ambalo huwa nalitoa kwa nadra sana.
"Tusikilize taarifa ya habari", nilimwambia.
Baada ya mlio wa tindo sauti ya kike ikasema.
"Sasa ni saa moja kamili". Halafu ikafuatiwa ya kiume.
"Ifuatayo ni taarifa ya habari kutoka Radio Tanzania Dar es Salaam msomaji Godfrey Chalamila. Kwanza habari kwa ufupi. Majasusi wawili walioshiriki katika njama za kuiba silaha za chama cha PLF bandarini wamekamatwa.
Mwili wa msichana mwanamapinduzi Veronika Amadu aliyeuawa katika harakati za kufichua njama za wizi wa silaha utasafirishwa kwenda Freetown, Sierra Leone.
Serikali imetaifisha makampuni yote yaliyokuwa chini ya Kampuni la kibepari la Euro-Afro.
Habari kamili; Wapelelezi shupavu wa Afrika jana usiku waliwakamata majasusi wawili na kuuwa wengine wengi na kuzikomboa silaha na kuzikomboa silaha za chama cha PLF zilizokuwa zimetekwa na majasusi waliokuwa wakiifanyia kazi Afrika Kusini. Majasusi hawa ni Ray Sikazwe, aliyekuwa rais wa chama cha SANP na Tonny Harrison aliyekuwa mwakilishi wa kampuni ya Euro-Afro.
Serikali imetamka kuwa watu hawa watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu kujibu mashitaka ya ujasusi na hujuma. Wakati huo huo kamati ya ukombozi ya OAU imelaani njama hizi za Makaburu na kusema kuwa lazima Makaburu wajue kuwa Afrika iko macho na haiko tayari kuchezewa. Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa chama cha PLF kitaongeza harakati za mapambano huko Afrika Kusini ambayo ndiyo njia pekee ya kuweza kupata uhuru wa walio wengi. Vile vile taarifa hiyo imesema kutakuwa na kikao cha kamati ndogo ya siasa mjini Dar es Salaam ili kutafuta njia ya kuviunganisha vyama vyote vya ukombozi vya Afrika Kusini, ili moto wa mapambano uweze kuwaka zaidi.
Mwili wa mwanamapinduzi shupavu hayati Veronika Amadu aliyeuawa katika harakati za kupambana na majasusi wa Makaburu ili kukomboa silaha zilizokuwa zimeibiwa bandarini utasafirishwa kwenda MJINI Freetown, Sierra Leon ambako ndiko kwao. Serikali imetoa ndege aina ya Boeng 737 ambayo itachukua na ujumbe wa kijeshi utakaosindikiza maiti hiyo pamoja na wanamapinduzi wengine. Imefahamika toka mjini Freetown kuwa mwanamapinduzi huyu atazikwa kwa heshima zote za kijeshi. Vyama vya wanamapinduzi na wapenda maendeleo duniani kote vimesema vitapeleka wawakilishi wao kwenye mazishi ya shujaa huyo.
Serikali imetaifisha makampuni yote yaliyokuwa chini ya kampuni ya kibepari ya Euro-Afro, kwa kile ilichokiita "Kujihusisha kwa kampuni hiyo na serikali ya Makaburu ili kupiga vita harakati za ukombozi. Hakuna fidia itakayotolewa. Na huo ndio mwisho wa taarifa ya habari".
Nilifunga radio baada ya taarifa ya habari maana ilinikumbusha Veronika.
"Utakwenda kwenye mazishi?", Zabibu aliuliza.
"Ndio".
"Tutakwenda wote?".
"Hamna taabu. Mambo yatatengenezwa.
TAMATI
BILA SHAKA UMEVUTIWA NA HADITHI HII YA UPELELEZI WA WIZI WA SILAHA ZA WAPIGANIA UHURU WA AFRIKA KUSINI, KAZI HII IMEFANYWA NA HAYATI E.A. MUSIBA AKITUMIA JINA LA WILLY GAMBA KAMA MPELELEZI HATARI WA AFRIKA. JIANDAE KUSOMA KITABU KIITWACHO 'UCHU'. KWA MAWASILIANO ZAIDI 0754296253, 0784296253, 0717522388.
KAKA TUWEKEE NA KIKOMO...HII NIMESHAISOMA YOTE....AU KIKOSI CHA KISASI.
ReplyDeleteThis comment has been removed by the author.
ReplyDeleteNice story mkuu ....shukrani
ReplyDeleteNzuri sana tunaomba ile ya mwadui
ReplyDeleteVipi ukitaka kukipata hiki kitabu inakuaje
ReplyDeleteVipi ukitaka kukipata hiki kitabu inakuaje
ReplyDeleteVp mkuu mi ndo kwanza naingia kwenye tovuti hii, na namshukuru mungu kwakuikuta hadith hii mahana nimeisaka sana,
ReplyDeleteila sijuw nifanyeje ili nipate mwanzo